TAMKO LA MWENYEKITI WA BODI

Mkataba wa Huduma kwa Mteja ni ahadi za kimaandishi kati ya Taasisi na wateja wake. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA) imetambua umuhimu wa kutumia Mkataba wa Huduma kwa Mteja kama mbinu ya kuleta mabadiliko chanya katika uwajibikaji wa watendaji wake kwa wateja. Hatua hii, inalenga kuboresha huduma inayotolewa na Mamlaka kwa wateja wakena wadau mbalimbali.


Kwa kuzingatia umuhimu wa jukumu lake kwa wateja na wadau mbalimbali, KASHWASA imeandaa Mkataba huu ambao unaainisha huduma inazotoa na viwango vya ubora wa huduma ambavyo wateja na wadau wana haki ya kupata. Pia, Mkataba huu umeweka wazi njia za kuwasiliana na Mamlaka na kueleza jinsi ya kupokea maoni au malalamiko na namna ya kuyashughulikia.


Nia ya KASHWASA ni kutoa huduma bora kwa wakati kulingana na viwango vilivyowekwa ndani ya Mkataba huu. Hivyo, mteja na mdau yeyote anashauriwa kusoma, kuelewa vizuri na kutumia ipasavyo Mkataba huu ili apate haki yake ya huduma bora.


Ninatambua kuwa kwa ujumla, KASHWASA imekuwa na mahusiano mazuri na wateja wake na wadau mbalimbali tangu ianze shughuli zake mnamo mwezi Februari 2009. Hivyo, nina imani kuwa Mkataba huu wa Huduma kwa Mteja utaimarisha mahusiano yetu mazuri na wateja na wadau mbalimbali katika utendaji na utoaji wa huduma. Aidha, nina imani kuwa Mkataba huu utakuwa kiungo muhimu cha mahusiano ya kikazi kati yetu na wateja. Kwa hiyo, ninawakaribisha wateja na wadau wetu wote kutoa maoni wakati wowote wanapojisikia kufanya hivyo ili nasi tuweze kuboresha huduma zetu.